Friday, June 15, 2012

Hatujadhamiria kupambana na umasikini nchini.


 Na: John Alex.

“Kama kila mmoja wetu angefagia nje kwake basi bila shaka dunia nzima ingekuwa safi”Haya ni maneno ya mtawa mmoja wa dini ya kikristo kutoka dhehebu la katoliki ajulikanae kwa jina la mama Theresa aliyewahi kuishi huko barani Asia nchini India,maneno ambayo leo nimeona nianze nayo.

Napenda sana kutumia mifano nikirejea maisha ya watu wa kipato cha chini ambao ndio walio wengi hapa nchini Tanzania hususan wakulima waishio maeneo ya vijijini na kama nikiwagusa   mijini basi napendelea wale waishio uswahilini maeneo ambayo ndio yanatoa taswira ya maisha halisi ya mtanzania.Achana na wale waishio mitaa ya  Masaki,Ostabei huko Dar es salaam,na kama ni mkoani Iringa basi waishio Wilolesi,na Igangilonga hawanihusu leo hii.

Bahatika siku moja kutembelea maeneo ya uswahilini,halafu kule chunguza kwa makini sana maeneo ambayo watu wanapenda kukusanyika wakiongea mambo mbali mbali,utapata majibu ambayo kwa sehemu fulani  yataendana na haya ya kwangu.

Uswahilini bwana,saluni za kiume  hufurika vijana ambao asilimia kubwa unawakuta wakisikiliza muziki wa kizazi kipya wala hawaendi kunyoa kwa sababu wengi wao utawaona na rasta kichwani.Hii iko sana  mijini tena utawakuta wengine maeneo ambayo wameyapa majina kama vile  kijiweni,kempu saiti na kadhalika na huko unawakuta wakiburudika na bangi ambayo imepewa majina  kama  vile Kaya,Widi,Mjani. na Ganja.

Kijjini  nako kuna wanaume wenye nguvu zao wasio na aibu ambao hawafanyi chochote na badala yake kuanzia asubuhi mwanzo mwisho utawakuta wakipiga mambo yetu yale,sasa kama ni hapa Iringa  au Mbeya ni Ulanzi ndio namaanisha.Kama  wangekuwa Ujerumani kipindi cha Adolf Hitler  wasomaji mashahidi watu kama  hawa ambao waliitwa kwa lugha ya kiingereza(unproductive) walikuswanywa vizuri tu na kutupwa baharini ama  walichomwa moto kwenye cchumba cha gesi.Na hii iliwatia adabu wajerumani wakati huo na matokeo yake nchi iliendelea na matokeo yake ikapata kiburi cha kuitawala dunia fuatilia historia  ya ujerumani.

Sasa huyu mwanamke  naye kaolewa na ni mama wa nyumbani,hana shughuli yeyote  ya kumuingizia kipato kamuandaa mumewe  kwenda kazini asubuhi ,kamvalisha mtoto tayari kumpeleka  kwenye kajinasari  jirani tu na nyumbani akisharudi mwanamke hatulizi miguu nyumbani asubuhi hiyo hiyo anasugua kisigino huyo! mpaka nyumba ya jirani,akifika kwa shoga yake wanatoa jamvi nje wanaanza kupeana michapo na mbaya zaidi  wengine wanavuka   mpaka mambo ya ndani  wanashea pamoja.Aaah! ndio mambo ya wanawake hayo. “Tutafanyaje na wakati huku mjini uswahilini nyumba zimebanana hata kufuga kuku tu ni inshu chumba chenyewe ni kimoja”Jamani hata  kuuza maandazi pia au kufuma vitambaa! kwani kuuza genge vipi?

Kwa mtazamo wangu nafikiri elimu ya uzazi wa mpango hususan baadhi ya maeneo  huko vijijini bado kabisa haijawafikia  na kama imewafikia basi hawajaielewa sawa sawa kwa sababu inakuaje  wanandoa wanazaa kila mwaka mtoto jamani? Inafikia kipindi familia unakuta ina watoto nane na kuendelea.Kibaya zaidi hembu kwa nje tu angalia afya ya mama na mtoto ilivyo ya kusikitisha! Mzee naye kachoka kweli kweli anategemea biashara ya mkaa na kuwalisha watoto na mama yao tu ni inshu siku nyingine wanashindia uji,nyumba ni ya nyasi tena wala dirisha haina na inakaribia kuanguka mchwa washafanya kazi yao.Kali zaidi watoto watatu wa mwisho  wana shinda  na chupi tu wengine ndio kidogo wana kaptura na wa kiume wakubwa  kidogo mashati ya baba yao ya zamani ndio wanajisitiri. Choo nacho kilishajaa siku nyingi na ukienda kusabahi hapo muda wowote angalia sana usije ukakanyaga kinyesi cha watoto.Kwa hili nasema watanzania  wote na serikali yetu  hatupo siriasi na hili swala

Huyu naye  anajiita sharobaro.Ni kijana, yuko stendi ya daladala na wala sio kuwa anasubiria Gari kaja kung’aa macho tu na kushangaa shangaa hana lolote.Anasogea kando ya barabara pembeni kidogo  kuna fundi viatu.Anaanza kucheka haalafu anasema; “Mimi bwana hata kama nimefika  darasa  la saba  kuna kazi nyingine  kufanya ni kama kujichoresha tu mchizi anashona viatu dah!kweli jamaa kauzu”

Hembu ona sasa hata darasa la saba naye katika ulimwengu huu wa leo anachagua kazi eti! Kama sio kunyonyana katika jamii ni nini huku.Kuna kauli ya wahenga inasema  mtembea bure si sawa na  mkaa bure. Sasa watu kama hawa  ambao wanaendekeza uvivu ikiwa hawana ujuzi wowote  na wala hawataki kuwa wabunifu,wala hawako tayari kujituma kufanya kazi kwa lengo la kuepuka kuwa  tegemezi  sikosei kuuita mzigo katika jamii  na serikali kwa ujumla.

Siku zote  ukitaka kutoa kibanzi  kilichoko ndani ya jicho la mwenzako basi ni vema na ni jambo la busara kama  ukianza kutoa boriti jichoni mwako kwanza na  kisha uanze sasa kukitoa cha huyo mwenzio.Namaanisha nini ?Ni kwamba wananchi wa Tanzania walio wengi tumekuwa tukiitupia lawama serikali pasipo kukumbuka  kuwa maendeleo katika taifa hili huletwa na wananchi wenyewe na serikali ni kama msimamizi tu.

Hapa msomaji naomba unielewe simaanishi kuwa serikali hawana mapungufu. Wanayo. tena makubwa tu.Usimamizi mbovu wa rasili mali nchini,ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi waliokosa uzalendo kwa taifa lao ambao wapo katika kutetea maslahi yao binafsi pasipo kujali  dhamana waliyopewa kuwatumikia watu  kwa kuzingatia  haki na usawa,pamoja na rushwa kubwa  iliyokithiri haya yote ni mzigo wa serikali.Sasa mimi leo nataka kila mmoja abebe mzigo wake hapa.

Vitabu vya dini karibia zote ulimwenguni  vimekuwa vikihimiza watu kufanya kazi kwa bidii na vingine vikiandika siri ya mafanikio ni   kujituma na kinyume na hapo huwezi kufanikiwa.Sasa kauli hii nayo inatoka katika Biblia,moja ya vitabu vya dini na inasema “Asiyefanya kazi na asile”

Leo nataka tuangalie umasikini kama tatizo la kijamii  na nafasi ya  jamii katika kupiga vita umasikini ambao madhara yake yamekuwa yakishambulia sana  jamii za  kitanzania  ambazo kwa nafasi yake pia jamii hizi zimekuwa zikijisahau kwa sehemu katika kulikabili tatizo aidha kutokana na kutojali ama kwa kukosa tu maarifa.Aidha mchango  anaoutoa mtu moja moja katika shughuli za kujiletea maendeleo unatolewa kikamilifu?
Umasikini kama tatizo la kijamii hugusa kila nyanja  katika maisha  ya binadamu ya kila siku.Hujumuisha  kipato kidogo kwa wanajamii,ukosefu wa huduma stahiki za kijamii kama vile maji umeme,hospitali,ukosefu wa mahitaji muhimu ya binadamu kama vile chakula mavazi na  malazi lakini pia  uwezo mdogo wa kufanya maamuzi  utokanao na  ujinga uliokithiri miongoni mwa jamii zetu za kitanzania,pia umasikini wa kiroho ambao humfanya mtanzania afikiri mawazo duni,awe ni mtu wa kukata tama,,na mwenye kujiona hawezi kufanya kitu chochote.

Asilimia kubwa mtakubaliana na mimi kuwa watanzania walio wengi katika jamii zetu tunamoishi  tumeshakata tamaa na tumeridhika kabisa na tulichonacho hata kama ni duni.Mbaya zaidi mwingine karidhika kabisa na  kukosa na hatimae kujikuta tukiishi maisha yasiyokuwa na muelekeo wowote kwani ni mara ngapi unakutana na watu waliokata tamaa na maisha  na wengi wetu tunafikiri hawa labda wamechanganyikiwa  kutokana na muonekano wao wa nje.Hii inatokana na uwezo duni wa kufanya maamuzi.

Kwa upande wavijana katika jamiii tunashindwa kuthubutu kufanya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine tunaamini kabisa kuwa  hatuwezi kutokana na mitazamo hasi ambayo imepandikizwa na waliotutangulia kwa maslahi yao.

Uvivu ni jambo ambalo linatawala vjana wengi wa kitanzania katika dunia hii ya leo na kushindwa kufanya  chochote  na ndio maana  matokeo yake tunashindwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa manuufaa yetu wenyewe.

Zipo fursa nyingi mitaani ambazo kwa  vijana ambao kutokana na sababu mbalimbali za msingi na zisizo za msingi wamekosa fursa ya kuendelea na masomo yaani wameishia  darasa la saba,ama  kidato cha nne wanaweza kuzitumia ipasavyo badala ya kuzidharau kujletea maendeleo ili kuepukana na tatizo kubwa la kuwa tegemezi.

Kwa akina mama ni muda muafaka sasa kuachana na mawazo na fikra mgando ambazo kwa maoni yangu zimepitwa na wakati.Fikra kama vile mwanaume peke yake ndiye mtafutaji mwanamke anabaki nyumbani.Na kwa wale dada zangu huu sio wakati wa kusubiria kuolewa kwani saasa hivi wanaooa wanatafuta mtu anayejituma na mchapa kazi,kinyume na hapo hutoolewa labdaumpate mvivumwenzio.Wakina dada tuepukane na hili tusije  tukaishia kufanya biashara za ajabu mtaani .Baadhi ya akina dada hawakawii.

Ni vema watanzania wakaeleweshwa kwa mapana juu ya hali halsi ya kiuchumi namabadilikoyanayotokea ulimwenguni kote.Katika kipindi hiki cha mabadiliko watanzania kila mmoja kwa nafasi yake atambue nafasiyake katika kuleta maendeleo,badala ya kutegemea serikali ambaayo na yenyewe  kwa kweli inakosa muelekeo kila kukicha

Tukumbuke kuwa sisi ni matunda ya kizazi kilichopita na sio wafungwa  wa kizazi kilichopita.Hivyo uwezo wa kuleta mabadiliko kuanzia ngazi ya familia kijiji  mkoa na taifa  upo mikononimwetu iwapo tu kila mmoja wetu kwa nafasi yake atashiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko.
Watanzania tukumbuke kuwa nchi nyingi ambazo leo hii ndio nchi wahisani,nchi zinazoitwa nchi zilizoendelea zilipita katika kipindi kigumu  kama hiki lakini baada ya kukubali matokeo na hatimae leo hii wanafaidi  matunda ya  juhudi zao.

Nijukumu letu sasa kuhakikisha kuwa tunaondokana na fikra za woga wa kuleta mabadiliko katika jamii,na badala yake tuvae ujasiri tukidhamiria kuleta  maendeleo katika nyanja zote katika taifa hili.

Yote haya yatafanikiwa endapo tutarejea na kuifanyia kazi kauli hii ya kila moja kufagia nje kwake na hatimae baadae tutajikuta tukiishi katika Tanzania yenye siasa safi,uongozi bora  na watu wote kunufaika na rasilimali za nchi na hivyo kupata fursa sawa kwa wote kattika kushiriki ujenzi wa taifa letu Tanzania





















             








Miundombinu ya kisasa itapandisha hadhi vyuo vyetu Iringa.




Na;John Alex.

Mwaka jana  nilibahatika kutembelea vyuo vikuu vya Mkwawa, Ruaha na Tumaini niliko sasa, hapa mkoani Iringa kujionea hali ya vyuo hivyo vinavyotoa elimu ya juu nchini.Sikupita kimya kimya ila nilipata fursa ya kuongea na baadhi ya wadau wa vyuo hivyo vikuu.

Kikubwa walichokizungumza wadau hawa ni pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili kama taasisi, lakini jambo kubwa walilotilia mkazo ni pamoja na miundombinu haba.Uhaba wa kumbi za kufanyia mihadhara, uhaba wa mabweni jambo ambalo kiukweli lilikuwa ni tatizo kubwa mno.Hawakuishia hapo wadau walieleza pia mikakati na mipango mbalimbali wanayoifanya kukabiliana na changasmoto zao huku wakitoa rai kwa taasisi hata zisizo za kiserikali kutoa misaada  katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili kama taasisi ya kijamii.

Ilikuwa ni jambo la ajabu sana lakini kwa hali halisi ya kitanzania hatushangai kwa sababu ndio tulivyo na ndio uwezo wetu.Kuna baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu hapa mkoania Iringa  wamekuwa wakielekezwa kuhudhuria vipindi katika kumbi za mikutano tena za watu binafsi ambazo hutumika kwa shughuli za harusi na sherehe kwa ujumla.Tumefanya kumbi za sherehe madarasa ya kufanyia mihadhara na tunalipa sawa na wanavyolipa wengine!Tutafanyaje na wakati hatujajipanga?

Wengine nao karibu asilimia 55 ya wanafunzi wanaishi nje ya chuo na huko nako ni dhahama tupu,mara huyu kaibiwa,mwingine kakabwa, sijasikia waliobakwa huenda wapo lakini  wanaona aibu kusema.Ni eneo hili hili wamelalamika kuwa maktaba iliyopo ni ndogo mno.Sasa mnasomea wapi? “Ahhh! tunajibana hivyo hivyo kwenye majani kama hivi tunalala kitabu kinakwenda si unajua mabenchi yenyewe machache”

Ni takribani mwaka mmoja hivi  umepita tangu nifanye dodoso zangu hizo,sasa nimepita tena hivi karibuni kuchunguza je ni kweli mipango  na mikakati niliyoambiwa inatekelezwa imefikia wapi na inaendeleaje.

Kiukweli sina budi kutumia kalamu yangu kupongeza  jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau hawa wa vyuo vikuu katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa miundombinu ya majengo.Wanajitahidi sana kwani wananchi wenyewe wanajionea kwa macho.

Ukienda Chuo kikuu Ruaha mjini pale utajionea namna ujenzi wa miundombinu unavyoendelea tena kwa kasi katika maeneo ya chuoni na hii ni katika kuhakikisha wanakabilina na changamoto yao ya uhaba wa kumbi za kufanyia mihadhara yao.Tutasoma kwenye kumbi za sherehe mpaka lini kama si kudidimiza hadhi ya elimu na chuo kwa ujumla?

Jengo kubwa la maktaba linaendelea  kupanda kwa kasi Chuo kikuu cha Mkwawa ili kukabilina na changamoto yetu ile ya kusomea kwenye mabenchi tena machache  kwani wengine  wanalala kwenye majani ndo wanasoma.Ni matumaini yangu kuwa hata mikakati ya ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi chuoni hapo imefikia pazuri tu,hapana shaka.Kwa nini wasifanye jitihada na wakati wamepewa zamana ya kusimamia na kuiendeleza taasisi?Ni kiongozi yupi asiyependa kusifiwa kwa kuendeleza  taasisi na kuifikisha pazuri.Ah!basi tu umasikini wetu huu ndio unatuponza.

Huku Tumaini nako mambo si mabaya kwani na wao wanajipanga kihaswa kukabiliana na tatizo hilo.Huku Tumaini kwa mujibu wa wanafunzi wenyewe wao wanasema  hawalilii sana kukaa ndani si unajua gharama wengine zinawashinda kwa hiyo mwaka mmoja ndani inayofwata yote nje !Ukisikia anayelilia kupata nafasi ya kukaa ndani basi ni mgeni huyo ndo kafika.Jengo la kisasa kabisa ujenzi unaendelea na kama inshalah panapomajaliwa likikamilika basi tutarajie kusikia tu bwana jamaa wameanzisha kitivo kipya.Kwani ni nani asiyependa maendeleo?

Hapa nchini kwetu si jambo la kushangaza sana kusikia taasisi Fulani ya elimu ya juu kulalamikia juu ya miundombinu chakavu nikimaanisha majengo pamoja na vitendea kazi kama magari na kadhalika  lakini muda muafaka unapofika sharti lazima tubuni mikakati kabambe ya kukabilinana na  matatizo yetu haya ambayo kimsingi sisi ndio chanzo.Kwani wanaozorotesha maendeleo si ni sisi wenyewe haswa pale tunaponyweshwa pombe na kupewa fulana na kofia halafu tunawachagua kwa hiari yetu kisha wakiharibu tunalalamika.

Sisi kama watanzania ni lazima tuhakikishe tunachukua hatua mbadala  hususan katika kuwachagua madereva wetu ambao tunaamini watatufikisha mahala sisi turidhike na kile wanachokifanya na hivyo tusijutie uamuzi wetu kama tunavyojuta baadhi yetu.Ni uamuzi huu pekee ndio utazifanya hata taasisi zetu za elimu ya juu zipige hatua katika kufikia malengo yake.

Sasa miundombinu ya kisasa katika vyuo vyetu hapa Iringa na nchi nzima kwa ujumla ni miongoni mwa mambo mazuri ambayo yanatarajiwa yangepewa kipaumbele sana kiasi ambacho kama ingefanyika hivyo basi tusingefika mahala tunalalamika  oohh! miundomibnu chakavu mara Gari la wagonjwa hakuna, hivi unafahamu kuwa yote hutegemea uongozi mzuri?

“Mbona vyuo vingine vinatoza ada kubwa halafu watu mmekaa kaa kimya tu kama wadudu fulani hivi!Tujiulize kwa makini je kodi wanayotozwa kama isingekuwepo sidhani kama serikali ingevumilia kitendo cha watu kupandisha ada kiholela.Kwa mtazamo wangu jibu ni hili; “Kama wangetufutia kodi kabisa  na tusilipe hata kidogo basi bila shaka sisi hatupendi dhuluma,tungeshusha ada mpaka kiwango cha chini kabisa.

Miundombinu imara ikiwemo madarasa ya kisasa yanatoa fursa kwa wasomi wetu kusoma kwa kujiamini zaidi,kusoma bila bugudhi yeyote na pia kuondoa kero ile ya kusoma huku watu wakiwa wamesimama kama ilivyo katika vyuo vyetu vikuu baadhi hapa nchini kama sio hapa hapa kwetu Iringa.

Saturday, January 21, 2012

Biashara zadorora chuoni Tumaini.




Na John Alex.

Baaadhi ya wafanya biashara wa vyakula wenye migahawa na wafanya biashara zingine wanaofanya shughuli zao za biashara maeneo ya chuo kikuu Tumaini  wamesema kuwa  katika msimu huu wa sikukuu   biashara ya vyakula na bidhaaa nyingine  maeneo hayo ya chuoni   imekuwa ngumu kupita kiasi.

Wakizungumza na Kwanza jamii kwa nyakati tofauti  wafanya biashara hao wamesema kuwa,  kufuatia likizo fupi  chuoni hapo wanafunzi ambao ndio wanunuzi wakuu wa vyakula  mahotelini na bidhaa nyingine  wamekwenda majumbani kwao kusherehekea sikukuu ya krismasi hali inayopelekea kudorora kwa biashara na wengine kuthubutu hata kuzifunga kabisa kwa muda.

“Asilimia kubwa ya  wateja wetu ni wanafunzi ambao wamekuwa wakinunua vyakula  mahotelini kwa hiyo wanapoondoka inatulazimu wakati mwengine kufunga kabisa hoteli zetu kwani  wanaobaki ni wachache ambao kati yao wapo wanaojipikia wenyewe” anasema Matata Elias .mmoja wa wafanya biashara mwenye mgahawa maarufu maeneo ya Tumaini ujulikanao kwa jina la Agape.

Aidha wafanyabiashra hao wamesema kuwa  biashara ya vyakula na bidhaa nyingine  maeneo hayo ya Tumaini huwa ni ya msimu ambapo wanafunzi wanapokuwa masomoni  biashara huwa inachanganya na pindi tu wafungapo  chuo  wao hulazimika  kufunga   na hivyo shughuli za biashara  kusimma kwa muda mpaka chuo kitakapofunguliwa.

Wafanya biashara hao wameongeza kuwa ugumu wa biashara chuoni hapo hususan kipindi hiki cha karibuni umechangiwa pia na kupanda kwa gharama za maisha  ambapo  wengi  wa wanafunzi inawalazimu kubana matumizi kwa kujipikia wenyewe.

“Hata hawa wachache waliobaki hawatuungishi vizuri kwa kweli nadhani ni kwa sababu ya uchache wao na wengi kuwa wamekwenda  likizo kwa hiyo  wengi wetu inatulazimu kufunga biashara zetu  kutokana na faida ndogo”anasema Hasani Lumato mmoja wa  wafanya biashra wanaojihusisha na ukaangaji wa chipsi.


Hata hivyo kwa upande wa biahsara nyingine kama vile  biashara za vifaa vya maofisini huwa ni kawaida yao pindi ifikapo muda wa likizo huwalazimu kufunga kabisa biashara zao kwani  wanafunzi na wafanya  kazi ambao ndio wanunuuzi wakuu wa bidhaa zao wanakuwa wamekwenda likizo na ambao wanabaki shughuli za masomo na kiofisi husimama.

Wanafunzi wa chuo cha Tumaini wamefunga likizo ndogo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya krismas  na  wanatarajia kurejea masomoni mara baada  ya sikukuu kuisha mwezi januari 2012.


Saturday, December 17, 2011

Mkuu wa wilaya Iringa ashauri ufugaji wa nyuki kisasa

Na John Alex.
           
Wananchi wa mkoa wa Iringa wameshauriwa kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu zaidi ili kuweza kujikwamua kutokana na hali ngumu  ya kimaisha na hivyo  kupiga hatua katika  vita dhidi ya umasikini na kujiletea maendeleo.

Hayo yamebainishwa  na mkuu wa wilaya ya Iringa mjini Asley Msangi katika kikao cha kamati ya ushauri (DCC)cha manispaa ya Iringa  kilichofanyika mwishoni mwa wiki ilyopita katika ukumbi wa manispaa ya Iringa.

Mkuu wa wilaya amesema kuwa wapo wananchi wanaoishi kwa kutegemea    ufugaji wa nyuki na hivyo ni vema wananchi wakaanzisha miradi ya  ufugaji nyuki kwa  njia za kisasa na za kitaalamu zaidi na hivyo kujipatia faida kupitia miradi hiyo.

Aidha mkuu wa wilaya ameishauri idara husika ya manispaa ya Iringa kuandaa mikakati madhubuti ya kuwezesha wananchi kujifunza namna ya kufuga nyuki  kwa njia za kisasa na za kitaalam zaidi na   hivyo kuweza kujipatia faida kubwa kutokana na  mazao ya nyuki.

“Wananchi endapo wataamua kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu wataweza kuinua zaidi kipato chao kwani mazao ya nyuki kama vile asali n anta yana soko sana na bei yake imekuwa ikipanda kila kukicha”alisema mkuu wa wilaya.

Amesema kuwa  ni wakati  muafaka kwa wananchi kuhamasika kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu zaidi na  kwa kushirikiana na idara husika  ya nyuki ya manispaa, kuhakikisha  kuwa miradi ya nyuki inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa  kwani ni njia mojawapo ya kuondokana na umasikini katika taifa letu.

Mkuu wa wilaya amesema kuwa  kwa muda mrefu idara husika ya nyuki ya manispaa ya Iringa  imekuwa  ikisuasua  sana katika  uhamasishaji wa miradi ya  ufugaji nyuki kwani kuna muitikio mdogo sana wa wananchi katika swala zima la ufugaji wa nyuki kwa wakazi wa manispaa ya Iringa

Ameishauri  idara hiyo ijifunze namna ya ufugaji nyuki kwa njia za kitaalamu na za kisasa na hivyo kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachi ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa zaidi ili kuwezesha wananchi wa manispaa ya Iringa wanaojihusisha na ufugaji wa nyuki kupata kwa wingi mazao ya nyuki na hivyo kujikwamua na umasikini.


Muitikio mdogo wa wananchi:Kikwazo kwa miradi ya waitaliano Iringa.

Na John Alex.

Muitikio mdogo wa wananchi wa  wa Iringa  katika shughuli za miradi mbalimbali zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoendesha shughuli zake kwa ufadhili wa watu wa Italia ni changamoto kubwa inayoyakabili mashirika hayo.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki katika maonyesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofadhiliwa na watu wa Italia waishio Mkoani Iringa yaliyofanyika katika hoteli  ya Wilolesi manispaa Ya Iringa.

Katika maadhimisho hayo ambayo yalikutanisha mashirika matatu  yanayofadhiliwa na waitaliano ambayo ni shirika la C.O.P.E(Coooperation for developing countries),shirika la Call Africa lenye miradi yake wilayani Iringa,na shirika la CUAM ambalo linafanya miradi yake mbalimbali ya afya mkoani Iringa.

Wadau wa miradi hiyo wamebainisha changamoto malimbali zinazowakabili katika  utendaji kazi wao huku wote wakilaumu muitikio mdogo hasa wa wananchi katika shughuli za miradi mbalimbali inayofanywa na mashirika yao.

“Kumekuwa na muitikio mdogo sana wa wananchi katika shughuli zinazofanywa na miradi mbalimbali ya shirika letu  la Call Africa kwa mfano akina mama wamekuwa wakikata tama katika kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kulelea watoto kama vile Kipepeo Nutritional  centre  ambavyo ni vya kutwa .Hali hii inawapa wakati mgumu wafadhili na ni changamoto kubwa”, anasema Lucas Marano msemaji wa  Call Africa.

Kwa upande wa shirika la CUAM  linalojihusisha na maswala ya afya msemaji  ambae alifahamika kwa jina moja  la Ricado amesema    kuna changamoto kubwa sana hasa katika upatikanaji wa wataalamu wa kutosha  katika kuendeleza program mbalimbali kaitka maeneo lengwa.

Aidha waitaliano hao wamebainisha changamoto nyingine zinazowakabili kuwa ni ushirikiano duni kutoka serikali kwani serikali imekuwa  ikijisahau katika kutoa ushirikiano wa kutosha hususan katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za zinazofanywa na miradi ya mashirika  hayo.

Tumeandaa mabango ya usafi katika program yetu ya USAFI rafiki wa maendeleo ,wenye lengo la  kuweka mji wa Iringa  katika hali ya usafi lakini kwa mara kadhaa tumekuwa tukicheleweshwa na wadau manispaa tunawaomba wasiwe wazungushaji katika suala zima la utekelezaji wa miradi ya maenddeleo anasema msemaji wa  Call Africa Lukas Marano.

Miradi mingine  inayofanywa na mashirika hayo matatu ukiiwemo mradiwa  kilimo MAWAKI na mengine mengineyo wamebainisha changamoto zinazofanana na kutaka wananchi wahamasike ili waweze kujikwamua na umasikini na kunufaika na miradi inayofanywa na mashirika haya.
Lengo la maadhimisho ni kutambulisha miradi ya waitalia wanaoishi Tanzania (wilaya za Iringa na Kilolo)kwa ajli ya watoto yatima ,walemavu,wenye mazingira magumu ,mafunzo kwa akina mama  na vijana,huduma ya afya, kilimo,mifugo,ujasiriamali,na  miango maalumu kuhusu UKIMWI

Thursday, December 15, 2011

MIAKA HAMSINI YA UHURU,TUTAMKUMBUKA RAIS KIKWETE KWA MIUNDOMBINU YA BARABARA.


.
Na John Alex.

Hivi karibuni watanzania tumeadhimisha miaka hamsini ya uhuru  ikiwa ni tangu  taifa hili lilipokombolewa kutoka katika mikono ya  waingereza mnamo tarehe 9  mwezi disemba  mwaka 1961 baada ya bendera  ya wakoloni  kushushwa pale kileleni mwa  mlima Kilimanjaro na kusimikwa kwa bendera ya  Taifa huru la Tanzania chini ya mwasisi baba wa taifa hayati Mwl.Julius  Kambarage  Nyerere ambaye kwa kushirikiana na  wanaharakati wenzie  walihakikisha kuwa taifa la Tanzania linakuwa huru na linatawaliwa na watanzania  wenyewe.

Katika maadhimisho hayo  yenye kauli mbiu ya  TUMETHUBUTU,TUMEWEZA ,NA  TUNAZIDI KUSONGA MBELE  wananchi  wamekuwa wakitafakari kwa kina sana juu ya kauli mbiu  hii kuwa ni nini tulichothubutu, ni nini tulichoweza na ni nini tunaendelea  kusonga nacho mbele.Wengi wana mawazo na mitazamo tofauti .Hii inawezekana ni kutokana na itikadi zao za kisiasa ama kutofautiana tu kimtazamo kutokana  na kile mtu anachoona na anachokiwaza kama sio anachokisikia.

Wasomi  na  wataalamu wa maswala mbalimbali  walioboboea katika kufanya tafiti mbalimbali nchini wamejaribu kutoa ripoti za utafiti waliofanya na kutoa tathmini ya kuhusu mafanikio yaliyopatikana  katika kipindi cha miaka hamsini  tangu taifa hili lipate uhuru.Tathmini hizo zimegusa katika  maeneo mbalimbali kama vile sekta ya afya, sekta ya elimu  na maeneo mengi ambayo wataalamu hawa wamekuwa wakifanyia tathmini
.
Hata hivyo kwa mujibu wa tathmini na ripoti mbalimbali za wataalamu hawa wa maswala  mbalimbali hapa nchini zimebainisha kuwa kiwango cha maendeleo kilichofikiwa hakilingani na umri wa miaka hamsini  ya Taifa hili tangu lilivyokuwa huru.Kwa mfano tunapoangalia sekta ya elimu hususani swala zima la ufaulu wa wanafunzi yaani kiwango cha elimu kwa ujumla kimeshuka  ukilinganisha na kipindi kilichopita.Tuachane  nahayo kwani  yanazidi kutukatisha tamaa

Ni dhahiri kuwa katika kipindi cha miaka yote hiyo ya uhuru hadi hivi leo,kuna mambo mengi ambayo  watanzania kiukweli tumethubutu, tumeweza na tunazidi kusonga mbele.Kwa hayo hatuna budi kujipongeza na pia kuipongeza serikali iliyopo maarakani kwa kujitahidi kuthubutu,kuweza na mpaka sasa tunazidi kusonga mbele.
Wahenga wana msemo unaosema,Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.Msemo huu una maana gani katika makala haya?Una maana kuwa,pamoja na mapungufu mengi tuliyoyaona na tuliyoyasikia kupitia vyombo vya habari kuhusu  serikali, yapo mambo mazuri ambayo serikali kimsingi imeyafanya na ni sharti tuipongeze kwa uthubutu na kuonyesha kuweza.Lakini pia tunapaswa kujipongeza sisi wenyewe kwani sisi ndio walipa kodi kwa hiyo  mafanikio hayo ni ya kwetu sisi hayainufaishi serikali peke yake
.
Leo  nitumie fursa hii kuwaomba watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa kuwa wakweli na wawazi hasa tunapoangazia katika swala zima la miundombinu ya barabara.Kwa wale  wazee wa mwaka sitini na moja  ni nani wakati ule alijua kuwa  angeweza kusafiri kutoka Tanga hadi Iringa kwa masasa nane  tu?Ni nani  wa wakati ule aliamini kuwa ipo siku Tanzania itaunganishwa na  barabara za lami kwa kila mkoa?Ni nani aliamini kuwa ipo siku barabara za lami zitafika hadi vijijni?Utakapofanya utafiti utagundua kuwa  wengi wahakuamini kuwa ipo siku Tanzania hii itakuwa na barabara  kuu nzuri zenye  kupendeza na zenye kiwango kinachotakiwa.
Leo hii kutoka  Dar es salaam hadi  Mbeya unahesabu masaa tofauti na kipindi kile  ambapo barabara hizi zilikuwa za vumbi na zenye kutisha na yeyote anayesafiri kati ya mikoa hiyo miwili afikapo mlima Kitonga basi roho mkononi na sala zote huzisalia hapo akihofia  kuwa huenda ndio mahala atakapofia kutokana na ubaya wa barabara iliyokuwepo kipindi kilichopita.

Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete  imethubutu ,imeweza na inazidi kusonga mbele katika swala la miundumbinu ya  barabara kwani hakuna awamu nyingine yeyote iliyopita ambayo imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha  miundombinu ya barabara zaidi ya awamu ya Rais Kikweteukweli ni huo.
Mikakati haiishii hapo tu bado ujenzi wa barabara za lami unaendelea kwa kasi ndani ya mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni barabara za kuunganisha wilaya ndani ya mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.Haya ni  mafanikio makubwa sana yaliyopatikana katika kipindi hasa cha awamu ya nne ya Rais Kikwete.Hapa turejee kauli mbiu yetu ya maadhimisho,TUNAZIDI KUSONGA  MBELE.
Leo wananchi kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha miundombinu ya barabara tuthubutu kusema kuwa tutamkumbuka  daima Rais Kikwete kwa kuimarisha miundombinu na si vinginevyo kwani hata kama kuna atakayefuata baada ya yeye bado yeye ndio atakuwa amefungua njia kuelekea mafanikio zaidi katika swala zima la miundombinu ya barabara.

Tukirejea hotuba ya Mh.Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya miaka hamsini ya uhuru katika viwanja  vya uhuru pale jijini Dar es  salaam kwa ufupi tu, alisisitiza  sana kuwa mafanikio yaliyopatikana katika swala zima la miundombinu ya  barabara nchini ni jambo kubwa sana la kujivunia kama taifa changa linaloendelea.

Rais Kikwete alibainisha  kuwa  hali ilvyokuwa  baada ya wakoloni kuondoka  kwa upande wa miundombinu ilikuwa si ya kuridhisha hata kidogo kwani barabara za lami zilikuwa chache kama hakuna kabisa.

  Hii ina maana   gani? Barabara chache zilizokuwepo zilikuwa ni kwa ajili ya kusafirisha malighafi kutoka kwenye maeneo ya mashamba hadi bandarini ili kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa hiyo  hazikulenga kamwe kuwanufaisha wananchi wa Tanzania bali wao wenyewe mabepari ambao walikuwa wakitunyonya
Lakini leo barabara za lami mpaka vijijini zinajengwa mfano hai ni mkoani Kilimanjaro ambapo baadhi ya barabara za vijini zimejengwa kwa kiwango cha lami sio tu Kilimanjaro bali na maeneo mengi sana ya Tanzania,  barabara za baadhi ya vijiji ni za kiwango cha lami.

Madaraja makubwa ya kuunganisha barabara hizi za kisasa yamejengwa na yaliyokuwa ya zamani yameimarishwa na kuwa ya kisasa.Mfano hai ni daraja la Mkapa lililojengwa katika kipindi cha mwishoni mwa wamu ya tatu ya Rais Mkapa, ambaloni daraja kubwa la mto rufiji.Achilia hilo kuna daraja la mto Ruvu ambalo limebadilishwa na kuimarishwa.

Ni wakati muafaka sasa baada ya kuadhimisha  miaka hamsini na kutafakari kwa kina juu ya mafanikio namapungufu yaliyopatikana katika miaka hamsini ya uhuru kuachana na  kutafakari mapungufu ,na kujikita zaidi katika  kujua ni kwa namna gani  sisi kama watanzania  tunafanya nini ili kutokomeza yale mabaya nakuendeleza zaidi mazuri yaliyofikiwa japo si kitu kwa baadhi ya watu wachache wenye maslahi binafsi na chuki dhidi ya taifa letu na serikaliiliyoko madarakani ka ujumla.

Aidha ni jukumu la serikali kusahihisha mapungufu yaliyokuwepo na  kuhakikisha kuwa inajipanga katika kuimarisha na kuboresha zaidi yale mafanikio mazuri ya kuridhisha  yliyofikiwa katika kipindi chote walichopo madarakani na pia kuendeleza juhudi za kuimarisha  mambo yote  yanayoihusu  kama serikali.

Pia ni jukumu la serikali kuhamasisha wananchi hususani maeneo ya kijijni kushiriki kiamilifu katika shughuli za kimaendeleo ambazo kimsingi ndizo zitalifanya taifa letu liendelee na kufikia katika kilele cha mafanikio.

Tuungane kwa pamoja katika  kupiga vita maadui wanaoliyumbisha taifa hilli ambao ni ujinga maradhi na umasikini uliokithiri miongoni mwa watanzania ambao kimsingi ndio vita kuu katika taifa letu.Miaka hamsini ya uhuru tuungane kwa pamija watanzania huku tukirejea kauli ya tumesubutu,tumeweza,na tunazidi kusonga mbele katika vita dhidi ya umasikini.MIAKA HAMSINI YA UHURU,TUMETHUBUTU TUMEWEZA,NA TUNAZIDI KUSONGA MBELE.

Wednesday, December 7, 2011

Baadhi ya bostani za mbogamboga zilivyoharibiwa na mafuriko Tumaini.