Na: John Alex.
“Kama kila mmoja wetu angefagia
nje kwake basi bila shaka dunia nzima ingekuwa safi”Haya
ni maneno ya mtawa mmoja wa dini ya kikristo kutoka dhehebu la katoliki ajulikanae
kwa jina la mama Theresa aliyewahi kuishi huko barani Asia nchini India,maneno
ambayo leo nimeona nianze nayo.
Napenda sana kutumia mifano
nikirejea maisha ya watu wa kipato cha chini ambao ndio walio wengi hapa nchini
Tanzania hususan wakulima waishio maeneo ya vijijini na kama nikiwagusa mijini
basi napendelea wale waishio uswahilini maeneo ambayo ndio yanatoa taswira ya
maisha halisi ya mtanzania.Achana na wale waishio mitaa ya Masaki,Ostabei huko Dar es salaam,na kama ni
mkoani Iringa basi waishio Wilolesi,na Igangilonga hawanihusu leo hii.
Bahatika siku moja kutembelea
maeneo ya uswahilini,halafu kule chunguza kwa makini sana maeneo ambayo watu wanapenda kukusanyika
wakiongea mambo mbali mbali,utapata majibu ambayo kwa sehemu fulani yataendana na haya ya kwangu.
Uswahilini bwana,saluni za
kiume hufurika vijana ambao asilimia
kubwa unawakuta wakisikiliza muziki wa kizazi kipya wala hawaendi kunyoa kwa
sababu wengi wao utawaona na rasta kichwani.Hii iko sana mijini tena utawakuta wengine maeneo ambayo
wameyapa majina kama vile kijiweni,kempu
saiti na kadhalika na huko unawakuta wakiburudika na bangi ambayo imepewa
majina kama vile Kaya,Widi,Mjani. na Ganja.
Kijjini nako kuna wanaume wenye nguvu zao wasio na
aibu ambao hawafanyi chochote na badala yake kuanzia asubuhi mwanzo mwisho
utawakuta wakipiga mambo yetu yale,sasa kama ni hapa Iringa au Mbeya ni Ulanzi ndio namaanisha.Kama wangekuwa Ujerumani kipindi cha Adolf
Hitler wasomaji mashahidi watu kama hawa ambao waliitwa kwa lugha ya kiingereza(unproductive)
walikuswanywa vizuri tu na kutupwa baharini ama
walichomwa moto kwenye cchumba cha gesi.Na hii iliwatia adabu wajerumani
wakati huo na matokeo yake nchi iliendelea na matokeo yake ikapata kiburi cha
kuitawala dunia fuatilia historia ya
ujerumani.
Sasa huyu mwanamke naye kaolewa na ni mama wa nyumbani,hana
shughuli yeyote ya kumuingizia kipato
kamuandaa mumewe kwenda kazini asubuhi ,kamvalisha
mtoto tayari kumpeleka kwenye
kajinasari jirani tu na nyumbani
akisharudi mwanamke hatulizi miguu nyumbani asubuhi hiyo hiyo anasugua kisigino
huyo! mpaka nyumba ya jirani,akifika kwa shoga yake wanatoa jamvi nje wanaanza
kupeana michapo na mbaya zaidi wengine
wanavuka mpaka mambo ya ndani wanashea pamoja.Aaah! ndio mambo ya wanawake
hayo. “Tutafanyaje na wakati huku mjini uswahilini nyumba zimebanana hata
kufuga kuku tu ni inshu chumba chenyewe ni kimoja”Jamani hata kuuza maandazi pia au kufuma vitambaa! kwani
kuuza genge vipi?
Kwa mtazamo wangu nafikiri elimu
ya uzazi wa mpango hususan baadhi ya maeneo huko vijijini bado kabisa haijawafikia na kama
imewafikia basi hawajaielewa sawa sawa kwa sababu inakuaje wanandoa wanazaa kila mwaka mtoto jamani?
Inafikia kipindi familia unakuta ina watoto nane na kuendelea.Kibaya zaidi
hembu kwa nje tu angalia afya ya mama na mtoto ilivyo ya kusikitisha! Mzee naye
kachoka kweli kweli anategemea biashara ya mkaa na kuwalisha watoto na mama yao
tu ni inshu siku nyingine wanashindia uji,nyumba ni ya nyasi tena wala dirisha
haina na inakaribia kuanguka mchwa washafanya kazi yao.Kali zaidi watoto watatu
wa mwisho wana shinda na chupi tu wengine ndio kidogo wana kaptura
na wa kiume wakubwa kidogo mashati ya
baba yao ya zamani ndio wanajisitiri. Choo nacho kilishajaa siku nyingi na
ukienda kusabahi hapo muda wowote angalia sana
usije ukakanyaga kinyesi cha watoto.Kwa hili nasema watanzania wote na serikali yetu hatupo siriasi na hili swala
Huyu naye anajiita sharobaro.Ni kijana, yuko stendi ya
daladala na wala sio kuwa anasubiria Gari kaja kung’aa macho tu na kushangaa
shangaa hana lolote.Anasogea kando ya barabara pembeni kidogo kuna fundi viatu.Anaanza kucheka haalafu
anasema; “Mimi bwana hata kama nimefika
darasa la saba kuna kazi nyingine kufanya ni kama kujichoresha tu mchizi
anashona viatu dah!kweli jamaa kauzu”
Hembu ona sasa hata darasa la
saba naye katika ulimwengu huu wa leo anachagua kazi eti! Kama
sio kunyonyana katika jamii ni nini huku.Kuna kauli ya wahenga inasema mtembea bure si sawa na mkaa bure. Sasa watu kama hawa ambao wanaendekeza uvivu ikiwa hawana ujuzi
wowote na wala hawataki kuwa
wabunifu,wala hawako tayari kujituma kufanya kazi kwa lengo la kuepuka
kuwa tegemezi sikosei kuuita mzigo katika jamii na serikali kwa ujumla.
Siku zote ukitaka kutoa kibanzi kilichoko ndani ya jicho la mwenzako basi ni
vema na ni jambo la busara kama ukianza
kutoa boriti jichoni mwako kwanza na
kisha uanze sasa kukitoa cha huyo mwenzio.Namaanisha nini ?Ni kwamba
wananchi wa Tanzania walio wengi tumekuwa tukiitupia lawama serikali pasipo
kukumbuka kuwa maendeleo katika taifa
hili huletwa na wananchi wenyewe na serikali ni kama msimamizi tu.
Hapa msomaji naomba unielewe
simaanishi kuwa serikali hawana mapungufu. Wanayo. tena makubwa tu.Usimamizi
mbovu wa rasili mali nchini,ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi waliokosa
uzalendo kwa taifa lao ambao wapo katika kutetea maslahi yao binafsi pasipo
kujali dhamana waliyopewa kuwatumikia
watu kwa kuzingatia haki na usawa,pamoja na rushwa kubwa iliyokithiri haya yote ni mzigo wa serikali.Sasa
mimi leo nataka kila mmoja abebe mzigo wake hapa.
Vitabu vya dini karibia zote
ulimwenguni vimekuwa vikihimiza watu
kufanya kazi kwa bidii na vingine vikiandika siri ya mafanikio ni kujituma na kinyume na hapo huwezi kufanikiwa.Sasa
kauli hii nayo inatoka katika Biblia,moja ya vitabu vya dini na inasema
“Asiyefanya kazi na asile”
Leo nataka tuangalie umasikini
kama tatizo la kijamii na nafasi ya jamii katika kupiga vita umasikini ambao
madhara yake yamekuwa yakishambulia sana
jamii za kitanzania ambazo kwa nafasi yake pia jamii hizi
zimekuwa zikijisahau kwa sehemu katika kulikabili tatizo aidha kutokana na
kutojali ama kwa kukosa tu maarifa.Aidha mchango anaoutoa mtu moja moja katika shughuli za
kujiletea maendeleo unatolewa kikamilifu?
Umasikini kama tatizo la kijamii
hugusa kila nyanja katika maisha ya binadamu ya kila siku.Hujumuisha kipato kidogo kwa wanajamii,ukosefu wa huduma
stahiki za kijamii kama vile maji umeme,hospitali,ukosefu wa mahitaji muhimu ya
binadamu kama vile chakula mavazi na
malazi lakini pia uwezo mdogo wa
kufanya maamuzi utokanao na ujinga uliokithiri miongoni mwa jamii zetu za
kitanzania,pia umasikini wa kiroho ambao humfanya mtanzania afikiri mawazo
duni,awe ni mtu wa kukata tama,,na mwenye kujiona hawezi kufanya kitu chochote.
Asilimia kubwa mtakubaliana na
mimi kuwa watanzania walio wengi katika jamii zetu tunamoishi tumeshakata tamaa na tumeridhika kabisa na
tulichonacho hata kama ni duni.Mbaya zaidi mwingine karidhika kabisa na kukosa na hatimae kujikuta tukiishi maisha
yasiyokuwa na muelekeo wowote kwani ni mara ngapi unakutana na watu waliokata
tamaa na maisha na wengi wetu tunafikiri
hawa labda wamechanganyikiwa kutokana na
muonekano wao wa nje.Hii inatokana na uwezo duni wa kufanya maamuzi.
Kwa upande wavijana katika jamiii
tunashindwa kuthubutu kufanya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine
tunaamini kabisa kuwa hatuwezi kutokana
na mitazamo hasi ambayo imepandikizwa na waliotutangulia kwa maslahi yao.
Uvivu ni jambo ambalo linatawala
vjana wengi wa kitanzania katika dunia hii ya leo na kushindwa kufanya chochote
na ndio maana matokeo yake
tunashindwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa manuufaa yetu wenyewe.
Zipo fursa nyingi mitaani ambazo
kwa vijana ambao kutokana na sababu
mbalimbali za msingi na zisizo za msingi wamekosa fursa ya kuendelea na masomo
yaani wameishia darasa la saba,ama kidato cha nne wanaweza kuzitumia ipasavyo
badala ya kuzidharau kujletea maendeleo ili kuepukana na tatizo kubwa la kuwa
tegemezi.
Kwa akina mama ni muda muafaka
sasa kuachana na mawazo na fikra mgando ambazo kwa maoni yangu zimepitwa na
wakati.Fikra kama vile mwanaume peke yake ndiye mtafutaji mwanamke anabaki
nyumbani.Na kwa wale dada zangu huu sio wakati wa kusubiria kuolewa kwani saasa
hivi wanaooa wanatafuta mtu anayejituma na mchapa kazi,kinyume na hapo
hutoolewa labdaumpate mvivumwenzio.Wakina dada tuepukane na hili tusije tukaishia kufanya biashara za ajabu mtaani
.Baadhi ya akina dada hawakawii.
Ni vema watanzania wakaeleweshwa
kwa mapana juu ya hali halsi ya kiuchumi namabadilikoyanayotokea ulimwenguni
kote.Katika kipindi hiki cha mabadiliko watanzania kila mmoja kwa nafasi yake
atambue nafasiyake katika kuleta maendeleo,badala ya kutegemea serikali ambaayo
na yenyewe kwa kweli inakosa muelekeo kila
kukicha
Tukumbuke kuwa sisi ni matunda ya
kizazi kilichopita na sio wafungwa wa
kizazi kilichopita.Hivyo uwezo wa kuleta mabadiliko kuanzia ngazi ya familia
kijiji mkoa na taifa upo mikononimwetu iwapo tu kila mmoja wetu
kwa nafasi yake atashiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko.
Watanzania tukumbuke kuwa nchi
nyingi ambazo leo hii ndio nchi wahisani,nchi zinazoitwa nchi zilizoendelea
zilipita katika kipindi kigumu kama hiki lakini baada ya kukubali matokeo na hatimae leo
hii wanafaidi matunda ya juhudi zao.
Nijukumu letu sasa kuhakikisha
kuwa tunaondokana na fikra za woga wa kuleta mabadiliko katika jamii,na badala
yake tuvae ujasiri tukidhamiria kuleta
maendeleo katika nyanja zote katika taifa hili.
Yote haya yatafanikiwa endapo tutarejea
na kuifanyia kazi kauli hii ya kila moja kufagia nje kwake na hatimae baadae
tutajikuta tukiishi katika Tanzania yenye siasa safi,uongozi bora na watu wote kunufaika na rasilimali za nchi
na hivyo kupata fursa sawa kwa wote kattika kushiriki ujenzi wa taifa letu
Tanzania
No comments:
Post a Comment