Thursday, December 1, 2011

Hatimae Mwanahabari Jerry Murro aachiwa huru.


 Aliyekuwa mtangazaji wa TBC  Jerry Murro akitoka nje ya mahakama baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili.(picha na www.globalpublisher.co.tz)




MAHAKAMA jijini Dar es Salaam, imewaachia huru aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa, baada ya kuonekana kuwa hawana hatia katika mashtaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili, likiwamo la kuomba rushwa ya Sh 10 milioni. 
Katika kesi hiyo ilikuwa inadaiwa kuwa Januari 29 mwaka jana, Muro na wenzake walitenda  makosa ya  kula njama, kushawishi kupewa rushwa ya Sh 10 milioni kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru. 

Hukumu iliyowaachia huru washtakiwa hao, ilisomwa jana saa 3:15 asubuhi na Hakimu Mkazi Frank Moshi  wa Mahakama ya Kisutu.

Hakimu huyo alisema mahakama imewaachia huru washtakiwa  baada ya upande wa mashtaka, kushindwa kuyathibitisha makosa pasipo kuacha shaka.  Katika shtaka la kula njama, Hakimu Moshi alisema  baada ya mahakama kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka, iliwaona washtakiwa  kuwa wana kesi ya kujibu na kuwataka kuwasilisha utetezi wao . 
Alisema hata hivyo baada ya kupitia ushahidi na utetezi uliotolewa na washtakiwa pamoja na ule wa shahidi wao mmoja (dereva wa Muro) katika shtaka la kula njama, mahakama imewaachia huru washtakiwa wote. 

 ”Mahakama imewaachia huru washtakiwa katika shtaka la kula njama kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa  kuithibitishia mahakama kama kweli washtakiwa walikutana na Wage na kufanya mawasiliano kupitia simu ya mkonon,” alisema hakimu Moshi.  Alisema mahakama imeona kuwa ushahidi wa nakala za picha za CCTV za hoteli ya Sea Cliff, zilizowasilishwa  na upande wa mashtaka zikionyesha watu watatu, sura zao zilikuwa hazionekani, jambo linalofanya ushahidi huo kuwa na upungufu. 

Hakimu huyo alisema ili  watu waweze kutenda kosa la kula njama lazima wawe wanafahamika na kwamba  hakuna ushahidi mwingine wowote  unaonyesha kuwa kweli washtakiwa hao walitenda kosa hilo.   Alisema upande wa mashtaka ulishindwa hata kumuita dereva wa Wage  ili aweze kuthibitisha kama kweli Wage na Muro waliwahi kuwa na mawasiliano au  kukutana katika Mgahawa wa Calfonia .

Alisema upande wa mashtaka pia ulishindwa hata kwenda kwenye makampuni ya simu ili kupata nakala za ujumbe mfupi wa simu (sms) waliokuwa wakitumiana Wage na Muro.

Alisema kitendo hicho kinaifanya mahakama isiamini kama kulikuwa na kosa la kula njama.  “Pamoja na kutokuwepo  kwa ushahidi wa mawasiliano pia upande wa mashtaka ulitakiwa upeleke mahakamani hati ya gwaride la utambuzi  ili kuithibitishia mahakama kama washtakiwa waliwahi kutambuliwa lakini hilo haliufanyika,”alisema hakimu Moshi. 
Katika shtaka la kuomba rushwa, hakimu Moshi alisema  mahakama haijaonyeshwa  ushahidi  wa kuthibitisha kuwa washtakiwa walipokea rushwa ya Sh 1 milioni  kutoka kwa Wage  kama kitangulizi  cha rushwa waliyoiitaji ya Sh10 milioni. 

Alisema mahakama ilitegemea kuwa kungekuwa na ushahidi wa mawasiliano au wa kuona ili kuonyesha uhalisia na kwamba eneo la Hoteli ya Sea Cliff,.

Aliongeza kuwa washtakiwa  Kapama na Mgasa walikamatwa katika maeneo tofauti tofauti, jambo liliosababisha mahakama kuwaachia huru hasa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka hilo.  Kuhusu shtaka  la kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru, linalokuwa likiwakabili Kapama na Mgasa, Hakimu Moshi alisema kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na vielelezo, hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa Wage aliwatambua washtakiwa hao katika gwaride la utambuzi. 
Alisema   vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka vinaonyesha kuwa mshtakiwa Mgasa alikiri kujitambulisha kuwa ni wafanyakazi wa TBC wakati katika maelezo ya mashahidi, inadaiwa kuwa walijitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru.

Alisema kwa msingi huo mahakama inawaachia huru washtakiwa hao kuwa shtaka hilo linajikanganya. 
“Washtakiwa wote wameachiwa huru  hata hivyo mahakama hii inazingatia kuwa kuna vielelezo kama risiti, pingu na bastola ambavyo havikuwa na mgogoro  hivyo virejeshwe kwa Muro. Na  kwa Yule  ambaye hajaridhika, haki ya kukata rufaa iko wazi,” alisema hakimu Moshi.  

Muro alipanda kizimbani Agosti 18 mwaka huu ambapo alijitetea na kuiomba mahakama  imuone kuwa hana hatia, akidai kuwa kesi inayomkabili ni ya kubambikiziwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi. 

Kesi hiyo ilipata hakimu mpya Frank Moshi Mei 2 mwaka huu  baada ya  Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe  kuhamishiwa katika Mahakama Kuu.Machi 8 mwaka huu hakimu huyo aliwaona washtakiwa hao kuwa wana kesi ya kujibu.Kwa kipindi chote hicho cha kusikilizwa kwa kesi hiyo washtakiwa wote walikuwa nje kwa dhamana kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment