Na John Alex.
Wananchi wa mkoa wa Iringa wameshauriwa kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu zaidi ili kuweza kujikwamua kutokana na hali ngumu ya kimaisha na hivyo kupiga hatua katika vita dhidi ya umasikini na kujiletea maendeleo.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya Iringa mjini Asley Msangi katika kikao cha kamati ya ushauri (DCC)cha manispaa ya Iringa kilichofanyika mwishoni mwa wiki ilyopita katika ukumbi wa manispaa ya Iringa.
Mkuu wa wilaya amesema kuwa wapo wananchi wanaoishi kwa kutegemea ufugaji wa nyuki na hivyo ni vema wananchi wakaanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu zaidi na hivyo kujipatia faida kupitia miradi hiyo.
Aidha mkuu wa wilaya ameishauri idara husika ya manispaa ya Iringa kuandaa mikakati madhubuti ya kuwezesha wananchi kujifunza namna ya kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalam zaidi na hivyo kuweza kujipatia faida kubwa kutokana na mazao ya nyuki.
“Wananchi endapo wataamua kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu wataweza kuinua zaidi kipato chao kwani mazao ya nyuki kama vile asali n anta yana soko sana na bei yake imekuwa ikipanda kila kukicha”alisema mkuu wa wilaya.
Amesema kuwa ni wakati muafaka kwa wananchi kuhamasika kufuga nyuki kwa njia za kisasa na za kitaalamu zaidi na kwa kushirikiana na idara husika ya nyuki ya manispaa, kuhakikisha kuwa miradi ya nyuki inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa kwani ni njia mojawapo ya kuondokana na umasikini katika taifa letu.
Mkuu wa wilaya amesema kuwa kwa muda mrefu idara husika ya nyuki ya manispaa ya Iringa imekuwa ikisuasua sana katika uhamasishaji wa miradi ya ufugaji nyuki kwani kuna muitikio mdogo sana wa wananchi katika swala zima la ufugaji wa nyuki kwa wakazi wa manispaa ya Iringa
Ameishauri idara hiyo ijifunze namna ya ufugaji nyuki kwa njia za kitaalamu na za kisasa na hivyo kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachi ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa zaidi ili kuwezesha wananchi wa manispaa ya Iringa wanaojihusisha na ufugaji wa nyuki kupata kwa wingi mazao ya nyuki na hivyo kujikwamua na umasikini.
No comments:
Post a Comment