Friday, June 15, 2012

Miundombinu ya kisasa itapandisha hadhi vyuo vyetu Iringa.




Na;John Alex.

Mwaka jana  nilibahatika kutembelea vyuo vikuu vya Mkwawa, Ruaha na Tumaini niliko sasa, hapa mkoani Iringa kujionea hali ya vyuo hivyo vinavyotoa elimu ya juu nchini.Sikupita kimya kimya ila nilipata fursa ya kuongea na baadhi ya wadau wa vyuo hivyo vikuu.

Kikubwa walichokizungumza wadau hawa ni pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili kama taasisi, lakini jambo kubwa walilotilia mkazo ni pamoja na miundombinu haba.Uhaba wa kumbi za kufanyia mihadhara, uhaba wa mabweni jambo ambalo kiukweli lilikuwa ni tatizo kubwa mno.Hawakuishia hapo wadau walieleza pia mikakati na mipango mbalimbali wanayoifanya kukabiliana na changasmoto zao huku wakitoa rai kwa taasisi hata zisizo za kiserikali kutoa misaada  katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili kama taasisi ya kijamii.

Ilikuwa ni jambo la ajabu sana lakini kwa hali halisi ya kitanzania hatushangai kwa sababu ndio tulivyo na ndio uwezo wetu.Kuna baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu hapa mkoania Iringa  wamekuwa wakielekezwa kuhudhuria vipindi katika kumbi za mikutano tena za watu binafsi ambazo hutumika kwa shughuli za harusi na sherehe kwa ujumla.Tumefanya kumbi za sherehe madarasa ya kufanyia mihadhara na tunalipa sawa na wanavyolipa wengine!Tutafanyaje na wakati hatujajipanga?

Wengine nao karibu asilimia 55 ya wanafunzi wanaishi nje ya chuo na huko nako ni dhahama tupu,mara huyu kaibiwa,mwingine kakabwa, sijasikia waliobakwa huenda wapo lakini  wanaona aibu kusema.Ni eneo hili hili wamelalamika kuwa maktaba iliyopo ni ndogo mno.Sasa mnasomea wapi? “Ahhh! tunajibana hivyo hivyo kwenye majani kama hivi tunalala kitabu kinakwenda si unajua mabenchi yenyewe machache”

Ni takribani mwaka mmoja hivi  umepita tangu nifanye dodoso zangu hizo,sasa nimepita tena hivi karibuni kuchunguza je ni kweli mipango  na mikakati niliyoambiwa inatekelezwa imefikia wapi na inaendeleaje.

Kiukweli sina budi kutumia kalamu yangu kupongeza  jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau hawa wa vyuo vikuu katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa miundombinu ya majengo.Wanajitahidi sana kwani wananchi wenyewe wanajionea kwa macho.

Ukienda Chuo kikuu Ruaha mjini pale utajionea namna ujenzi wa miundombinu unavyoendelea tena kwa kasi katika maeneo ya chuoni na hii ni katika kuhakikisha wanakabilina na changamoto yao ya uhaba wa kumbi za kufanyia mihadhara yao.Tutasoma kwenye kumbi za sherehe mpaka lini kama si kudidimiza hadhi ya elimu na chuo kwa ujumla?

Jengo kubwa la maktaba linaendelea  kupanda kwa kasi Chuo kikuu cha Mkwawa ili kukabilina na changamoto yetu ile ya kusomea kwenye mabenchi tena machache  kwani wengine  wanalala kwenye majani ndo wanasoma.Ni matumaini yangu kuwa hata mikakati ya ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi chuoni hapo imefikia pazuri tu,hapana shaka.Kwa nini wasifanye jitihada na wakati wamepewa zamana ya kusimamia na kuiendeleza taasisi?Ni kiongozi yupi asiyependa kusifiwa kwa kuendeleza  taasisi na kuifikisha pazuri.Ah!basi tu umasikini wetu huu ndio unatuponza.

Huku Tumaini nako mambo si mabaya kwani na wao wanajipanga kihaswa kukabiliana na tatizo hilo.Huku Tumaini kwa mujibu wa wanafunzi wenyewe wao wanasema  hawalilii sana kukaa ndani si unajua gharama wengine zinawashinda kwa hiyo mwaka mmoja ndani inayofwata yote nje !Ukisikia anayelilia kupata nafasi ya kukaa ndani basi ni mgeni huyo ndo kafika.Jengo la kisasa kabisa ujenzi unaendelea na kama inshalah panapomajaliwa likikamilika basi tutarajie kusikia tu bwana jamaa wameanzisha kitivo kipya.Kwani ni nani asiyependa maendeleo?

Hapa nchini kwetu si jambo la kushangaza sana kusikia taasisi Fulani ya elimu ya juu kulalamikia juu ya miundombinu chakavu nikimaanisha majengo pamoja na vitendea kazi kama magari na kadhalika  lakini muda muafaka unapofika sharti lazima tubuni mikakati kabambe ya kukabilinana na  matatizo yetu haya ambayo kimsingi sisi ndio chanzo.Kwani wanaozorotesha maendeleo si ni sisi wenyewe haswa pale tunaponyweshwa pombe na kupewa fulana na kofia halafu tunawachagua kwa hiari yetu kisha wakiharibu tunalalamika.

Sisi kama watanzania ni lazima tuhakikishe tunachukua hatua mbadala  hususan katika kuwachagua madereva wetu ambao tunaamini watatufikisha mahala sisi turidhike na kile wanachokifanya na hivyo tusijutie uamuzi wetu kama tunavyojuta baadhi yetu.Ni uamuzi huu pekee ndio utazifanya hata taasisi zetu za elimu ya juu zipige hatua katika kufikia malengo yake.

Sasa miundombinu ya kisasa katika vyuo vyetu hapa Iringa na nchi nzima kwa ujumla ni miongoni mwa mambo mazuri ambayo yanatarajiwa yangepewa kipaumbele sana kiasi ambacho kama ingefanyika hivyo basi tusingefika mahala tunalalamika  oohh! miundomibnu chakavu mara Gari la wagonjwa hakuna, hivi unafahamu kuwa yote hutegemea uongozi mzuri?

“Mbona vyuo vingine vinatoza ada kubwa halafu watu mmekaa kaa kimya tu kama wadudu fulani hivi!Tujiulize kwa makini je kodi wanayotozwa kama isingekuwepo sidhani kama serikali ingevumilia kitendo cha watu kupandisha ada kiholela.Kwa mtazamo wangu jibu ni hili; “Kama wangetufutia kodi kabisa  na tusilipe hata kidogo basi bila shaka sisi hatupendi dhuluma,tungeshusha ada mpaka kiwango cha chini kabisa.

Miundombinu imara ikiwemo madarasa ya kisasa yanatoa fursa kwa wasomi wetu kusoma kwa kujiamini zaidi,kusoma bila bugudhi yeyote na pia kuondoa kero ile ya kusoma huku watu wakiwa wamesimama kama ilivyo katika vyuo vyetu vikuu baadhi hapa nchini kama sio hapa hapa kwetu Iringa.

No comments:

Post a Comment