Na John Alex.
Wananchi wa kijiji cha Kigonzile kilichopo kata ya Nduli Manispaa ya Iringa ,wameiomba serikali isaidie kiwango kinachotakiwa kuchangiwa na wananchi hao ili kijiji hicho kiweze kuletewa maji kupitia mradi wa maji wa benki ya dunia,baada ya kushindwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni kumi na moja walizotakiwa kutoa kama mchango wa wananchi.
Akizungumza na Kwanza jamii,mwenyekiti wa kijiji hicho, Joackim Muonge,amesema kuwa serikali iliwataka wananchi wa kijiji hicho kuchangia kiasi cha shilingi milioni kumi na moja kama sharti la benki ya dunia pindi inapotaka kusaidia miradi ya maendeleo lakini mpaka sasa kiasi hicho cha fedha hakijatosheleza kwani mpaka sasa wananchi hao wameweza kukusanya kiasi cha shilingi laki nne na themanini 480000 tangu mwezi wa tano mwaka jana.
Amezitaja sababu zinazochangia wanakijiji hao kushindwa kutoa kiasi cha fedha ya mchango huo kwa ajili ya mradi huo wa benki ya dunia kua ni pamoja na uwezo mdogo kiuchumi kwa wanakijij hao ambapo asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji chake ni wajane na hawana shughuli ya kuweza kuwaingizia kipato kizuri ,kukabiliana na majukumu ya kimaisha kama vile kusomesha watoto shule za sekondari sambamba na kuzidiwa na michango mingine ya kimaendeleo kama vile ujenzi wa shule ya sekondari kijijini hapo.
“Tumeanza rasmi kukusanya michango tangu mwaka jana mwezi wa tano ambapo mpaka sasa ni shilingi laki nne na themanini tu ndio zimeshakusanywa”alisema mwenyekiti .
Aidha mwenyekiti huyo amebainisha kuwa uhaba wa mvua hasa katika kipindi hiki cha kiangazi umechangia kwa kiasi kikubwa sana upatikanaji wa maji kuwa wa shida kwani chemchemi chache zinazotegemewa na wanakijiji kutoa walau maji safi nazo zimekauka na hivyo kubakia na chanzo kimoja tu cha maji ambacho ni mfereji wa Mchambawima ambao nao maji yake si salama japo wanalazimika kuyatumia maji hayo kutokana na uhaba wa maji unaowakabili.
“Wanakijiji wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa wa kuhara mara kwa mara kutokana na kutumia maji ya mfereji huo ambayo sio maji safi wala salama kwani mfereji huu unakotoka wanaelekezea mabomba ya majitaka ambayo humwaga uchafu humo”
Kwa upande wa wananchi kijini hapo,wameliambia kwanza jamii kuwa: “tatizo la maji hapa kijijini limekuwa sugu, kwani kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitusahau sana katika kutatua tatizo zima la maji jamani tunaiomba serikali itufikirie tunataabika kwa muda mrefu sana kutokana na kipato kidogo na uwezo wetu duni” anasema mmoja wa wanakijiji,Petro Sila.
Aidha kwa upande wake Angelo Lukinga, mkazi wa kijijini hapo ameiomba serikali iwape kipaumbele wanakijiji wa kigonzile ili waweze kuondokana na kero sugu ya maji ambayo inawasumbua kwa muda mrefu na kuwafanya wataabike na kuandamwa na maradhi ya kuhara.
Wanakijiji wa kijiji cha Kigonzile wamebainisha changamoto nyingi zinazokikabili kijiji chao ikiwa ni pamoja na ukosefu wa zahanati ndogo ya kijiji, barabara mbovu, na ukosefu wa umeme lakini wamelitaja tatizo la maji kama changamoto kubwa sana inayowakabili kijijini hapo.
No comments:
Post a Comment